Ijumaa, 20 Mei 2016

ALAMA ZA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI ZITATUMIKA KATIKA TAASISI ZA SERIKALI

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Mindi Kasiga, akiongea na waandishi wa habari kwenye mkutano uliofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere, ambapo alizungumzia matumizi ya Alama za Jumuiya ya Afrika Mashariki ambazo ni Bendera na Wimbo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika Taasisi za Serikali.

Mkurugenzi wa Masomo katika Chuo cha Diplomasia Dkt. Watengere Kitojo (kushoto) pamoja na Afisa Mawasiliano wandamizi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Robi Bwiru.
Bi. Mindi Kasiga akiendelea kuzungumza na Waandishi wa Habari.

Mkurugenzi wa Masomo katika Chuo cha Diplomasia, Dkt. Watengere Kitojo naye akizungumza kuhusu zinazotolewa na chuo hicho ikiwemo Cheti, StaShahada, Shahada katika masuala ya Uhusiano wa Kimataifa

Sehemu ya Waandishi wa habari waliojitokeza kwenye mkutano huo, katikati ni Afisa kutoka Habari Maelezo Bi. Immaculata Makilika akifuatilia kwa makini mkutano.

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inatoa wito kwa Taasisi za Serikali kuhakikisha kuwa zinatumia alama za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambazo ni Bendera na Wimbo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Alama hizo zinatakiwa kutumika kwenye Ofisi za Serikali (Wizara, Idara zinazojitegemea, mashirika ya umma na Wakala) sambamba na alama za Taifa yaani 

Bendera ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Wimbo wa Taifa.
Bendera ya Jumuiya inatakiwa kupepea sambamba na Bendera ya Taifa kwenye Ofisi za Serikali na Wimbo wa Jumuiya nao unatakiwa kuimbwa sambamba na Wimbo wa Taifa wakati wa shughuli rasmi za Kiserikali.

Hatua hiyo ni utekelezaji wa Mkataba wa Uanzishwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambao katika kifungu cha 7(a) umesisitiza Jumuiya hii kuwa ni Jumuiya ya watu, hivyo wananchi wa Tanzania watahusishwa katika hatua zote za Mtangamano. 

Aidha, Serikali ya awamu ya tano (5) chini ya Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki itahakikisha kuwa Watanzania wanashirikishwa kikamilifu katika hatua mbalimbali za Jumuiya ili kuijua kwa madhumuni ya kunufaika na fursa mbalimbali zinazopatikana ndani ya Jumuiya hiyo.

Matumizi ya alama hizi ni njia mojawapo ya kujenga uzalendo na kumfanya Mwananchi ajisikie kuwa sehemu ya Ushirikiano huu. Aidha, Taasisi binafsi hasa Mashule na Vyuo wanasisitizwa kutumia alama hizi kama sehemu ya kuelimisha na kuhamasisha vijana kuhusu Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki itaratibu zoezi la upatikanaji wa sampuli ya alama hizo kwa gharama za taasisi husika, hivyo Wizara, Taasisi na Ofisi za Serikali zinahimizwa kuwasiliana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa ajili ya ufafanuzi zaidi wa upatikanaji na matumizi ya alama hizo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Ad Inside Post