Jumanne, 23 Agosti 2016

LAWRENCE MAFURU: KUNA MASHIRIKA YA UMMA YANAYOLIPIWA MISHAHARA NA HAZINAA

Na John Banda, Dodoma

MSAJILI wa Hazina,Lawrence Mafuru amekiri kuwa bado kuna msururu wa mashirika ya umma ambayo kila siku yanapanga foleni Hazina kwaajili ya kusaidiwa huku mengine yakisaidiwa kulipiwa mishahara ingawa yanafanya biashara.


Kauli hiyo aliitoa jana katika kikao cha Kamati ya bunge ya hesabu za serikali(PAC) ilipokuwa ikihoji hoja za Mkaguzi Mkuu wa hesabu za serikali(CAG) kwa benki ya posta Tanzania, mjini hapa.


Mafuru alisema kwasasa  inajidhihirisha na kuondoa hisia kuwa mashirika ya umma yanayomilikiwa na serikali hayawezi kuendeshwa kwa ufanisi. 


Alibainisha licha ya hisia hizo lakini bado Hazina kuna msururu wa mashirika yanayosaidiwa ingawa yanajiendesha kibiashara.


“Lakini hapa tunapata ushahidi tukiyasimamia vizuri mashirika yetu na kuyasaidia yanaweza kujiendesha na kuleta tija na kupata faida,”alisema Mafuru


Hata hivyo alisema kwa jitihada zilizofanywa na benki ya posta inapeleka meseji kwa mashirika mengine kwamba hakuna kisingizio inawezekana kujiendesha kwa ufanisi na tija.


Alisema maagizo  yaliyotolewa na kamati hiyo yatasaidia benki ya posta kufikia malengo yake.

“Benki iendelee kujiimarisha na kuyafanya mashirika mengine yatakayoingia kwenye kamati ya PAC kujipanga na kuonesha kwa namna gani inaweza kuwasaidia watanzania kwa kujiendesha kwa faida kupitia miradi ya maendeleo, naipongeza Benki hii kwa sasa kujiimarisha tofauti na ilipokuwa mwanzo,”alisema Msajili huyo


Alibainisha benki hiyo kwasasa ipo kibiashara na ipo kwenye nafasi ya juu kati ya zaidi ya benki 50 na kwamba taasisi kama hizo kwasasa zinatakiwa kujiendesha kibiashara na kuyataka mashirika mengine kujifunza katika hilo.


Mafuru alisema inawezekana kujiendesha na kutengeneza faida badala ya kuwa tegemezi na hivyo utamaduni huo uigwe na mashirika mengine.


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Aeshi Hilaly, aliipongeza benki hiyo kwa kufikia mtaji wa sh. Bilioni 41 ambapo alisema ilikuwa kwenye mtaji wa chini sana hapo awali na kuonekana ikielekea kufa.


Naye Mwenyekiti wa bodi ya benki hiyo, Profesa Lettice Rutashobya, alisema atashughulikia mapungufu yaliyojitokeza katika ukaguzi ili mwaka ujao kusiwe na hoja hizo.


Aidha alisema atahakikisha benki hiyo inajiimarisha na hatarudi katika hali iliyokuwa awali kutokana na mikakati iliyopo ikiwa ni pamoja na kufunga mifumo mbalimbali ili kuwa na uwezo wa kushindana na benki zingine.



Mwisho.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Ad Inside Post